Takht Ravanchi ameandika katika mtandao wa X: "karibuni hivi nimerejea kutoka Abu Dhabi. Katika duru ya kwanza ya mashauriano ya kisiasa kati ya nchi mbili, nilikuwa na mazungumzo marefu na yenye tija kubwa na Lana Nusseibeh, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Muungano wa Falme za Kiarabu".
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na Masuala ya Kisiasa ameongezea kwa kusema: "nilikutana pia na kufanya mazungumzo na Khalifa Shaheen, Waziri wa Nchi anayehusika na Mambo ya Nje na Anwar Gargash, Mshauri wa Kidiplomasia wa Rais wa Imarati. Katika mikutano yote tuliyofanya, pande mbili zimeonyesha hamu ziliyonayo ya kupanua uhusiano, hususan katika uga wa kiuchumi".
Takht Ravanchi ameendelea kueleza katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X: "majirani wana nafasi maalumu katika sera zetu za nje. Kupitia urafiki na ushirikiano, tunaweza kujenga mustakabali bora na wa mafanikio zaidi kwa ajili ya eneo letu".
Kikao cha kwanza cha Kamati ya Pamoja ya Mashauriano ya Kisiasa kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Muungano wa Falme za Kiarabu kilifanyika Abu Dhabi Ijumaa, Februari 28. Katika kikao hicho, ambapo Majid Takht Ravanchi na Lana Nusseibeh, waliongoza jumbe za nchi zao mbili, pande mbili za Tehran na Abu Dhabi zilijadiliana na kubadilishana mawazo juu ya masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano wa nchi mbili yakiwemo ya kisiasa na kiuchumi. Kuchunguza matukio ya kikanda na kimataifa ilikuwa ajenda nyingine iliyotawala mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Katika kikao hicho, sambamba na Takht Ravanchi kusisitizia umuhimu wa utaratibu unaoandaliwa na Kamati ya Pamoja ya Mashauriano ya Kisiasa na nafasi yake katika kusaidia kuimarisha uratibu ili kuendeleza uhusiano wa pande mbili na kubadilishana mawazo juu ya matukio ya kikanda na kimataifa, alisema, anatumai kwamba, kwa kufanya vikao vyao kwa utaratibu wa kudumu, pande mbili za Iran na Imarati zitaweza kuongeza kasi ya utekelezaji wa makubaliano ziliyofikia na kubaini fursa nyingine mpya za ushirikiano.
Safari ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini Imarati imefanyika katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa kupatikana usalama endelevu na ustawi wa kieneo kutawezekana tu kupitia ushirikiano na ushirikishwaji wa nchi zote jirani. Madola ya kigeni yasiyo na uhusiano wowote na eneo hili yanapinga kuwepo uhusiano wa kirafiki kati ya Iran na nchi jirani; na hivyo yanaendeleza chokochoko za kuzusha migogoro kwa lengo la kuvuruga usalama na utulivu.
Pamoja na hayo, Tehran inaendeleza juhudi zake za kuwa na uhusiano bora zaidi na majirani zake, ambapo kudumisha uhusiano wa kipekee na nchi jirani ikiwemo Imarati kuna umuhimu maradufu kwa Iran. Mikakati na diplomasia ya Iran katika eneo la Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi imejengeka juu ya msingi wa kutilia mkazo udharura wa kutumia uwezo wa kikanda na wa ndani ya nchi za eneo hili kwa ajili ya uendeshaji wake; na Tehran inaamini kwa dhati kuwa uingiliaji wa maajinabi na madola ya kigeni katika uga huo si kwa maslahi ya nchi za eneo hili.
Kwa kutegemea nguvu na uwezo wake wa ndani, Iran imeweza kudhamini usalama wa baharini katika Ghuba ya Uajemi na Mlango Bahari wa Hormuz, jambo linalodhihirisha nafasi na mchango muhimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kudhamini utulivu na amani ya eneo.
Katika sera zake za nje, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka pia kuwepo na utulivu na usalama na kuwa na uhusiano bora na majirani zake. Uhusiano mwema kati ya Iran na majirani zake, mbali na kuwa na faida katika nyanja za kiuchumi, una umuhimu wa kimkakati pia kwa ajili ya kudumisha usalama wa pamoja katika eneo hili.
Uhusiano wa aina hiyo unafungua njia ya kubadilishana uwezo na fursa za kiuchumi, biashara na uwekezaji kati ya majirani, jambo ambalo bila shaka lina manufaa kwa nchi zote za eneo hili. Pande haribifu na zinazoingilia masuala ya eneo hili zinaelewa vyema kwamba, matokeo yasiyo na shaka ya kuboreshwa uhusiano kati ya Iran na majirani zake yatakuwa ni kuimarika usalama wa eneo bila ya kuhitajia madola ya kigeni na kustawishwa ushirikiano baina ya pande mbili na baina ya pande kadhaa katika nyanja zote.
Sera ya Iran kuhusiana na usalama katika eneo hili inafuata mwongozo wa kuwa na amani na usalama wa pamoja; na kwa msingi huo, Tehran inaamini kuwa kuvurugika usalama katika eneo hili ni kwa madhara ya nchi zote za eneo. Kutokana na hali iliyopo hivi sasa katika eneo hili kuna haja ya kulipa kipaumbele suala la kufanya mazungumzo na kuwepo maelewano ili kutatua tofauti zilizopo kati ya nchi jirani.
Ziara ya Takht Ravanchi mjini Abu Dhabi imejikita katika kufuatilia malengo ya sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kupanua uhusiano na nchi za Ghuba ya Uajemi. Katika miaka ya karibuni, Iran imekuwa na uhusiano mkubwa wa kiuchumi na Imarati; na kwa kuzingatia uwezo na fursa za kiuchumi zilizonazo nchi hizo mbili, kuna uwezekano wa kuongezwa zaidi mashirikiano ya pande mbili.
Kipaumbele cha Iran katika ushirikiano wake na majirani zake daima kimekuwa ni kuzingatia maslahi ya pande zote mbili. Iran na nchi jirani zina anuai za fursa za pamoja za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kwa ajili ya kuwa na mahusiano na maelewano mazuri baina yao.../
342/
Your Comment